Hamasa mpya ya itakayokusaidia kudumu katika mahusiano ya kimapenzi

Mapenzi ni kitu cha tofauti kidogo. Umeshawahi kuona watu wakiwa ndani ya mapenzi moto moto? Umeshaona wanavyokuwa wakiwa pamoja? Hata kama wana miaka sitini ila wakati mwingine huwezi kuwatofautisha matendo yao na watoto wadogo.

Hapo ndipo mapenzi yanapohitaji nafasi yake ili uweze kuyaelewa vizuri. Mapenzi yana lugha ya ajabu sana, wakati unapoweza kumjibu rafiki yako “poa tu, haina noma, haya bhana na maneno mengine kama hayo ” na isilete matatizo ila katika mapenzi hapa ni lazima utengeneza vita ya tatu ya dunia. Hapo mwenzako anaweza kuhisi umekasirika, anaweza kudhani sasa hivi humuheshimu kama zamani  ilmradi tu. Hapo ndipo mapenzi yanapohitaji nafasi zaidi.

Kila unachofanya kwa mpenzi wako kina maana kubwa hata kama hujadhamiria. Unapopokea simu haraka anapokupigia inaleta maana fulani kwake hata unapochelewa pia anapata maana. Tofauti ni moja tu, pale atapata maana nzuri kuwa unamjali na kumuheshimu wakati huku atapata maana hasi- inayoweza kumpa wasi wasi na katika nafsi yake. Katika mapenzi hakuna kitu kidogo!

Simu yako kwake ina maana, sms yako ina maana hata aina ya utani unaomletea pia unamletea tafsiri fulani katika akili yake. Kuna utani mwingine ukimfanyia anajiuliza mmmh… ni utani huu? Au kafikisha ujumbe kwa namna tofauti? Hayo ndiyo mapenzi ambayo yanamfanya mpenzi wako akuombe salio na ukimtumia yote anatumia kuongea na wewe, tena ukiangalia kwa haraka unaweza kusema hakuna neno la maana alilokwambia.

Ila kujua kitendo cha kukupigia simu tu kwake na kwako pia kina maana kwa sababu kukupigia simu ni faraja kubwa kwa sababu kaongea na mtu anayemuamini na kumkabidhi hisia zake. Mtu ambaye ana mamlaka ya kumuuliza jana kwanini ulichelewa kulala ama kwanini leo umevaa hivi.

Mtu wa kipekee aliyeamua kumruhusu kuwa na neno juu ya maisha yake. Hayo ndiyo mapenzi, Anakupigia mara kwa mara si kwa sababu hana watu wengine wa kuongea nao hapana. Ni kwa kuwa anakujali na kukuthamini. Ukiona suala hilo ni dogo basi mwenzako ataona humthamini wala kumjali. Ataona unamdharu, Ataona anajipendekeza kwako.

Unajua matokeo ya fikra za namna hiyo zikimea katika kichwa chake? Ni kujiona hayuko na mtu sahihi katika maisha.

Thamini kila unachofanyiwa na mwenzako bila kuangalia ukubwa wala thamani yake. Katika mapenzi kila jambo lina nafasi yake ya kuyajenga ama kuyabomoa mahusiano yenu. Ukiona kumpigia sana simu ni usumbufu, we acha tu. Ukiona kumwita majina ya kimapenzi mwenzako si kitu, sawa tu. Ila unapaswa kukaa tayari kwa matokeo ya bomu unalotengeneza. Ukae vizuri pale mwenzako atakapokwambia ama kuwaeleza marafiki zake humjali wala humthamini.

Vijengavyo mapenzi ya kweli si magari na kupelekana ‘out’ Dubai tu ila ni kila jambo la kimapenzi ulifanyalo kwa mwenzi wako bila kujali ukubwa wala thamani yake.
Thamani ya tendo unalomfanyia mwenzako litaamuliwa na kiwango cha hisia alicho nacho juu yako nafsini kwake. Kama mtu hana hisia na wewe hata umfanyie nini atafurahi na kukuona wa kawaida tu ama mwenye pesa sana. suala ni hisia. Mapenzi ni hisia.

Na mwenye hisia na wewe kila jambo kwake ni muhimu. kauli ndogo tu zimeweza kurejesha amani na upendo katika nyumba nyingi, pia kauli zingine ambazo pia ni ndogo zimesababisha nyumba nyingi kuvunjika. Kuwa makini na matendo na kauli zako kwa mwenzako. Hakuna kidogo katika mapenzi. Kila jambo lina thamani yake

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *